Dar es Salaam. Ni simulizi ya Hellena Silas, mwanzilishi na mkurugenzi wa Kampuni ya Arena Recycling, inayojihusisha na urejelezaji taka za plastiki kutengeneza vifaa vya ujenzi kama matofali na mbao mbadala.
Bidhaa hizi zinatumia taka za plastiki na mchanganyiko wa malighafi nyingine.
Kinachofanyika ni ushuhuda wa jinsi mawazo ya ubunifu, juhudi na mapenzi ya kweli kwa mazingira yanavyoweza kubadilisha dunia na kutengeneza fursa mpya kwa jamii.
Ubunifu wa Hellena unafanyika wakati ambao takwimu zinaonyesha takriban tani milioni nane za plastiki hutupwa baharini kila mwaka duniani.
Ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ya mwaka 2021 inaonyesha plastiki huchangia asilimia 85 ya takataka za baharini na inakadiriwa kiwango cha uchafuzi wa plastiki kitaongezeka maradufu kufikia mwaka 2030.
Safari ya Hellena katika kupunguza tatizo hili ilianza mwaka 2020 akiwa mgeni jijini Dar es Salaam alikofika kwa ajili ya masomo akitokea mkoani Mbeya alikozaliwa, kukua na kusoma hadi ngazi ya sekondari.
Kabla ya kufika jijini Dar es Salaam, alivutiwa kutembelea maeneo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi kutokana na picha alizoona kupitia runinga.
Hata hivyo, alipofika jijini alistaajabu, kile alichokiona na kuvutiwa nacho hakikuwa kama kilivyo katika uhalisia.
Badala ya fukwe safi alikuta chupa nyingi za plastiki na takataka nyingine za baharini (marine waste) zikielea majini.
Kwa mujibu wa Hellena, hali hii ilimfanya kujiuliza mengi: “Kwa nini hatuna miundombinu sahihi ya kutunza taka hizi? Je, hakuna mamlaka zinazoshughulikia mazingira haya?”
Hali hii ilikuwa mwanzo wa wazo jipya kwake, aliamua kutafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo.
Akiwa mhitimu wa shahada ya utaalamu wa maabara, aliachana na kile alichosoma, akitumia ubunifu akatumia plastiki hizo kama fursa.
Hellena alianza kuchunguza jinsi wengine duniani walivyoshughulikia masuala ya uchafuzi wa mazingira na walichofanya kutunza fukwe na mazingira kwa jumla.
Baada ya kutafiti aligundua baadhi ya nchi wanachakata taka na kuzigeuza kuwa rasilimali za nishati au mafuta na kuna hata faini kwa wale ambao wanakataa kuzingatia kanuni.
Hellena aliona hiyo ni njia nzuri ya kupunguza uchafuzi wa mazingira. Alijiuliza kwa nini hilo halifanyiki Tanzania?
Alibaini hapakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu uchakataji wa taka, lakini alikuwa na matumaini anaweza kuwa sehemu ya mabadiliko.
Akiona uchakataji taka za plastiki unaweza kuwa suluhisho, Hellena akapata ndoto ya kuanzisha mradi wa kuchakata plastiki na kugeuza kuwa vifaa vya ujenzi.
Jambo hilo lilimfanya ajifunze zaidi kuhusu urejelezeshaji, akagundua ni jambo kubwa na kwa mataifa mengine ni biashara inayozalisha mapato mengi.
Pia, alijua uchakataji taka za plastiki unaweza kuwa fursa ya kipekee na ya manufaa kwa mazingira.
Hakutaka kusubiri, badala yake aliamua kuanzia kazi nyumbani kwa kutumia masufuria, kipindi hicho walikuwa hawajapiga marufuku mifuko ya plastiki kwa hiyo aliitumia kama kufanya majaribio.
“Nilitumia Sh300,000 kutengeneza chemba kwa ajili yakutengenezea matofali, nilitumia mkaa na kuni kuchemsha na zote zilikuwa kwa ajili ya mfano,” anasema.
Ingawa safari ilikuwa ngumu, hakukata tamaa, badala yake aliongeza juhudi akaona mabadiliko.
Alianza kupata ushirikiano kutoka kwa watu wengi ambao waliona wazo lake, walivutiwa na hatua yake ya kufanya jambo.
Katika uzalishaji anasema kilo moja ya chupa hutoa tofali ndogo (pavement) saba hadi 10 ukilinganisha na aina ya umbo. Kwa tofali kubwa hutoka mbili. Anaeleza tani moja ya chupa inatoa matofali 300.
Bidhaa zake zilipoanza kuonekana kwa wateja ziliongeza uhitaji, ingawa changamoto za uzalishaji zilikuwapo, ikiwamo kukosa mashine za kutosha kwa ajili ya kuzalisha bidhaa nyingi.
“Tulipoanza tulikuwa na mashine inayoweza kusaga kilo 300 hadi 500 kwa siku, baadaye tulipata inayosaga chupa za plastiki tani tano hadi saba kwa siku iliyogharimu Sh11.5 milioni. Kwa upande wa mashine ya kuchanganya na kutoa tofali tulikuwa na ile yenye uwezo wa kuzalisha matofali 300 kwa siku,” anasema.
Kufanyia kazi nyumbani ni moja ya jambo lililowazuia kuwa na vitu vingi, kwani eneo lilikuwa dogo.
“Ilikuwa ngumu sana kupata mashine inayoweza kuleta kila kitu ambacho tunakitaka, lakini kwa sasa tuna mashine yenye uwezo wa kuzalisha vifaa vya kisasa,” anasema.

Hellena alijua huu ni mwanzo, baadaye alifungua kiwanda kidogo cha kuchakata plastiki na sasa ameongeza bidhaa nyingine ya mbao mbadala (WPS).
“Kwa sasa tuna kiwanda kikubwa ambacho kina uwezo wa kubeba tani 100 za plastiki na tumeongeza bidhaa zetu sokoni.
“Tukitangaza bidhaa zetu huwa tunapata shida kwa sababu wateja wakiwa wengi sana tunazidiwa katika uzalishaji,” anasema.
Kupitia kile wanachokifanya wamefanikiwa kufanya miradi ya ujenzi kwa majengo madogo kwa kujenga matundu ya vyoo katika shule mbalimbali.
Miongoni mwa miradi waliyofanya na wanaikumbuka ni kujenga matundu 14 ya vyoo katika Shule ya Msingi Buza iliyopo Manispaa ya Temeke.
Pia, wamekamilisha ujenzi wa matundu manane ya vyoo na chumba cha wasichana cha kubadilishia nguo wanapokuwa katika hedhi kwenye Shule ya Msingi Karume.
Mradi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Karume ulikuwa chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.
Hadi sasa kina mama 30 wanafanya kazi katika eneo hilo kusaidia uzalishaji wa matofali, huku wengi wakinufaika kwa kukusanya taka za chupa katika maeneo mbalimbali ya jijiji na kuziuza kwake.
WPS (Wood Plastic Substitution) ni bidhaa ya ujenzi inayotumika kama mbadala wa mbao. Inatengenezwa kwa mchanganyiko wa plastiki iliyochakatwa na nyenzo nyingine kama vile mkaa ili kutengeneza bidhaa zinazofanana na mbao.
Bidhaa hiyo hutumika katika maeneo mbalimbali ya ujenzi, kama vile sakafu, kuta na kuweka muundo wa nje wa majengo.
Pia, katika kutengeneza samani za nje kwa sababu ina sifa za kustahimili maji na kuoza kuliko mbao za kawaida.
WPS hutumika kama suluhisho kwa shida ya upungufu wa mbao na ni njia nzuri ya kutumia taka za plastiki kwa kuzibadilisha kuwa bidhaa zenye manufaa. Bidhaa hizo hutumika pia kupunguza uchafuzi wa mazingira.